
Waziri wa zamani wa Utumishi wa Umma, Justin Muturi, amemkosoa Rais William Ruto kwa agizo lake kwa polisi kuwapiga risasi waandamanaji wanaokiuka sheria, akisema ni matumizi mabaya ya mamlaka na usaliti kwa Katiba.
Muturi alisema agizo hilo ni hatari na isiyowajibika, akiitaja kama kielelezo cha ukosefu wa huruma na kichocheo cha unyanyasaji wa polisi dhidi ya raia.
Kauli yake ilikuwa kwenye taarifa yenye kichwa “Urais Unaosaliti Katiba: Wakati wa Aibu kwa Ruto,” iliyotolewa usiku wa manane Ijumaa, Julai 11, 2025.
“Rais William Ruto alisimama mbele ya taifa linalougua. Taifa lililo katika maombolezo ya vifo vya vijana wake waliouawa kwa risasi kikatili, taifa lililotaka si msaada bali heshima," Muturi alisema.
"Na katika wakati huo muhimu ambapo uongozi ulitaka busara, huruma na mshikamano, Rais alichagua vitisho na kutishia. Aliwaambia polisi ‘mpigeni tu mguuni.’ Agizo la kizembe, lisilojali maisha ya binadamu, ambalo halitakumbukwa kama matamshi ya bahati mbaya, bali doa kwenye roho ya Jamhuri hii,” aliongeza.
Muturi alihusisha pia kauli hiyo ya Ruto na mwenendo mpana wa ukatili wa serikali, akitaja agizo la awali la Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen, aliyewataka polisi “wawakabili waandamanaji kwa ukatili.”
Kwa mujibu wa Muturi, kauli kama hizo zinawatia moyo maafisa wa polisi wasioheshimu sheria na kuhatarisha utawala wa sheria.
Akinukuu Ibara za 26, 27, 28, na 29 za Katiba, Spika huyo wa zamani wa Bunge la Taifa alisema matamshi ya Ruto yamekiuka haki za msingi, hasa haki ya kuishi, usawa, heshima ya binadamu na kinga dhidi ya mateso au adhabu ya kikatili au ya kudhalilisha.
“Kinachotia wasiwasi zaidi ni kwamba agizo hili la uchochezi lilikuja baada ya maelekezo mengine ya vitisho kutoka kwa Waziri Kipchumba Murkomen, aliyewataka polisi wawashughulikie waandamanaji kwa ukali.
"Wakati wale walio kwenye kilele cha mamlaka ya dola wanapotumia nafasi zao kuhalalisha ukatili, wanawatia nguvu wanaokiuka sheria katika taasisi zinazopaswa kuwalinda raia. Matamshi haya kutoka kwa Rais na Waziri wake si tu ya kuchukiza kimaadili; ni ukiukaji wa Katiba,” alisema.
“Tuwe wazi: Kauli ya Rais Ruto inakiuka moja kwa moja Ibara ya 26, 27, 28, na 29 za Katiba ya Kenya. Ibara ya 26 inalinda haki ya kuishi. Rex Masai, Eric Ochieng na Kenneth Onyango – hawa si majina tu; ni watoto wa taifa hili ambao haki yao ya kuishi ilikatizwa kwa risasi zilizodhaniwa kuhalalishwa na kauli ya Kiongozi wa Taifa.”
Muturi alikataa jaribio lolote la kuhalalisha matamshi ya Rais kwa kisingizio cha usalama wa taifa, akisema usalama wa kweli hujengwa kwa imani, mazungumzo na utawala wa kikatiba, si kwa hofu.
Alionya kuwa Kenya inashuhudia kurudi kwa mwenendo wa kiimla, ambapo maandamano yanachukuliwa kuwa uhalifu na sauti za upinzani kukabiliwa kwa nguvu za mauti.
Ruto: Wapigeni Risasi Miguuni Waandamanaji Wanaopora Badala ya Kuwaua
“Urais huu unaonekana kuwa na nia ya kuhalalisha matumizi ya polisi kama silaha dhidi ya wananchi wanaokosoa. Matokeo yake ni kupungua kwa nafasi ya kidemokrasia na kuzoeleka kwa ukatili wa dola. Inapaswa kuwatia wasiwasi Wakenya wote, bila kujali msimamo wao wa kisiasa, kuwa Rais ambaye awali alitetea uhuru wa polisi sasa anatumia mamlaka yake kutoa maagizo ya kiutendaji ambayo ni sawa na amri za kiharamu,” Muturi alisema.
Alimtaka Rais Ruto kufuta kauli hiyo mara moja na kuwaomba msamaha hadharani familia za waathiriwa wa ukatili wa polisi, akionya kuwa kutochukua hatua kutaharibu zaidi hadhi ya urais.
Muturi pia aliwakumbusha maafisa wa polisi kuwa wameapa kuilinda Katiba, si kutekeleza maagizo haramu — jukumu ambalo lina uzito wa kisheria kitaifa na kimataifa.
“Rais Ruto lazima afute kauli yake mara moja na kutoa msamaha wa hadharani kwa familia za waliouawa na kujeruhiwa na polisi waliochochewa na maneno yake. Kwa kufanya hivyo, lazima athibitishe kuwa serikali italinda – si kuwinda – raia wake,” ilisoma taarifa hiyo.
“Polisi pia wanapaswa kukumbushwa kuwa kiapo chao ni kwa Katiba, si kwa mtu binafsi. Kutii maagizo haramu, hasa yanayosababisha kuua raia kinyume cha sheria, kunawafanya wawajibike kibinafsi chini ya sheria za Kenya na sheria za kimataifa.”