
Nairobi, Kenya, Julai 21 — Mwanaharakati Boniface Mwangi ameachiliwa kwa dhamana ya Sh1 milioni na Mahakama ya Hakimu ya Kahawa, Nairobi.
"Mshtakiwa anaweza kuachiliwa huru baada ya kupata dhamana ya kibinafsi ya Sh1 milioni pamoja na mdhamini mmoja wa kiwango sawa," alisema Hakimu Mkuu Gideon Kiage katika uamuzi wake.
Mawakili wa Mwangi wametaka kesi hiyo ihamishwe hadi Mahakama ya Milimani kwa kuwa mashtaka yaliyopo hayausiani tena na ugaidi.
Mwangi alishtakiwa kwa kosa la kupatikana na risasi bila cheti halali cha kumiliki silaha, na alikana mashtaka hayo mbele ya mahakama.

Mawakili wa utetezi, akiwemo Makamu wa Rais wa Chama cha Wanasheria wa Kenya (LSK), Mwaura Kabata, walitaka mahakama imwachilie kwa dhamana ya kibinafsi au masharti ya dhamana ya haki.
"Mshtakiwa ni mwanaharakati aliyethibitishwa na mtetezi wa katiba yetu," alisema wakili Ndegwa Njiru.
Wakili huyo aliongeza kuwa mshtakiwa si mtu wa kukimbia kesi, ni raia anayeheshimu sheria, na makazi pamoja na biashara yake vinajulikana kwa maafisa waliomkamata.
Aidha, mawakili waliiomba mahakama kuhamisha kesi hiyo hadi Mahakama ya Milimani kufuatia kuondolewa kwa mashtaka ya ugaidi dhidi ya mshtakiwa.
Kesi hiyo itatajwa tena ndani ya siku 14 kwa ajili ya maelekezo ya awali ya usikilizaji.
Awali, Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) iliondoa mashtaka ya ugaidi dhidi ya Mwangi yaliyokuwa yametangazwa kufuatia kukamatwa kwake siku ya Jumamosi.
Mwangi alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu ya Kahawa ambapo alitarajiwa kukabiliwa na mashtaka ya ugaidi kama ilivyotangazwa na DCI siku ya Jumapili.
Alikamatwa nyumbani kwake Lukenya, Kaunti ya Machakos, na maafisa kutoka DCI waliodai kwamba kukamatwa kwake kulihusiana na madai ya ushiriki wake katika uratibu na kuwezesha vitendo vinavyochukuliwa kuwa vya kigaidi chini ya Sheria ya Kuzuia Ugaidi.

Wapelelezi walisema walipata vifaa vya kielektroniki na nyaraka kadhaa wakati wa msako nyumbani kwake.
Pia walidai kupata mizinga miwili ya gesi ya machozi ambayo haikutumika kutoka ofisi yake ya Mageuzi Hub, Hurlingham, pamoja na risasi moja tupu ya 7.62mm.
Vitu vingine vilivyopatikana ni diski ngumu tisa za nje, kompyuta mpakato mbili, mihuri ya kampuni za Brave Media Ltd na Courage Ltd, mhuri mmoja wa kampuni, vitabu sita vya hundi, na nakala za nyaraka za ushuru wa mihuri.
Mamlaka ilidai kuwa Mwangi alihusika kikamilifu katika uratibu na ufadhili wa maandamano ya Juni 25, ambako watu kadhaa waliuawa, mali ya umma kuharibiwa, na maafisa wa usalama kujeruhiwa.
Alizuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Pangani, Nairobi.
Wakili wake, Njanja Maina, siku ya Jumapili alikanusha madai ya kupatikana kwa mizinga ya gesi ya machozi na risasi tupu, akisema hayo ni madai ya uongo yaliyolenga kumshtaki kwa ugaidi.

