
NAIROBI, KENYA, Alhamisi, Novemba 20, 2025 – Mwenyekiti wa Chama cha Orange Democratic Movement (ODM), Oburu Oginga, amefichua kwamba aliwahi kumwonya kaka yake, marehemu Raila Odinga, kuhusu hatari ya ugomvi wa kifamilia kuhusu urithi wa mali na uongozi wa kisiasa.
Akizungumza na gazeti moja la humu nchini, Oburu alisema masuala ya muda mrefu yanayohusiana na mali na usimamizi wake yalikuwa “bomu iliyotegwa” ndani ya familia ya Odinga, ikisubiri tu siku ya kulipuka.

Anasema mazungumzo hayo yalifanyika kwenye simu, zikiwa zimesalia siku chache tu kabla ya Raila kufariki nchini India mnamo Oktoba 15.
Kwa mujibu wake, walikuwa tayari wamepanga kikao cha kukutana Dubai mnamo Oktoba 19 ili kuhitimisha suala hilo. Lakini mauti yakamkuta Raila kabla hawajafika mezani.
Oburu anasema alimwambia kaka yake bila kupindisha maneno:
“Maliza suala la urithi sasa. Hakikisha kila mtoto na ndugu anapata chake. Usiache chochote kitakachogeuka chanzo cha vita baadaye,” Oburu alimwambia Raila.
Aliongeza kuwa aliogopa kizazi kipya huenda kisiwe na mshikamano kama ule aliokuwa nao na Raila.
“Maisha ni mafupi,” alimwambia Raila. “Kikitokea kwako au kwangu kabla tumalize haya, hawa vijana hawatashikana kama sisi.”
Kisha janga likatokea — Raila akaaga dunia.
Mazishi yake ya haraka ndani ya saa 72, kama alivyoagiza, yaliupiga taifa huzuni nzito. Umati mkubwa ulijitokeza Nairobi, Kisumu na Bondo.
Lakini nyuma ya machozi… nyufa zikaanza kuonekana.
Winnie Acharuka Mbele Ya Umma : Asema Vigogo Wanataka “Kuuza ODM”
Mpasuko ulilipuka hadharani kwenye sherehe za ODM@20 huko Mombasa.
Winnie Odinga, bintiye Raila, alivuruga utulivu kwa madai makali kwamba baadhi ya vigogo wanapanga kukiuza chama alichokijenga baba yake.
Vyanzo vya karibu na familia vinadokeza kuwa hasira hiyo imetokana na wiki kadhaa za mvutano ndani ya familia.
Ilikuwa dhahiri kwamba mambo hayako sawa Winnie alipokosa kuhudhuria hafla ya kumtawaza kaka yake, Raila Junior, kama msemaji wa familia.
Halafu mlipuko ukatokea rasmi kwenye jukwaa la Mama Ngina Waterfront.
Chanzo kikuu cha mgongano ni nafasi ya ODM ndani ya serikali jumuishi — mpango ambao Raila aliunga mkono kabla ya kufa.
Winnie anaamini mpango huo unaharibiwa. Oburu anasisitiza huo ndiyo ulikuwa msimamo wa mwisho wa Raila.

Kauli Yake Winnie Yapandisha Joto Kwa Viongozi wa ODM
Akihutubia umma, Winnie alishambulia uongozi wa ODM kwa kejeli nzito, akisema mpango huo “ni mgumu na mzito” na zamani ulitegemewa akili na busara ya Baba.
Aliitaka kuitishwa kwa Mkutano Mkuu (NDC) ili wanachama waamue ni nani anayefaa kusimamia uhusiano wa ODM na serikali.
Baadhi ya maafisa wa ODM walimshutumu kwa kumvunjia heshima Dr Oburu kwenye jukwaa.
Lakini Oburu alibaki mtulivu. Alikumbusha umma kuwa yeye ni mwanzilishi wa ODM na alikuwa sambamba na Raila katika kila hatua ya safari yake ya kisiasa.
Kisha akamwambia Winnie kwa utulivu: Masuala ya familia yatashughulikiwa nyumbani — si kwenye majukwaa ya kampeni.




© Radio Jambo 2024. All rights reserved