

Mkutano wa Viongozi wa Dunia kuhusu Wanawake unaofanyika
jijini Beijing ni fursa ya dhahabu kwa nchi duniani kote kubadilishana uzoefu
na kuendeleza uwezeshaji wa wanawake, amesema afisa mmoja wa serikali ya Misri.
Kabla ya kuhudhuria mkutano huo unaotarajiwa kufanyika
Jumatatu na Jumanne, Amal Amaar, Rais wa Baraza la Kitaifa la Wanawake nchini
Misri (NCW), aliambia shirika la habari la Xinhua kwamba hafla hiyo itakuwa
jukwaa muhimu kwa washiriki kutathmini mafanikio, kushiriki changamoto na
kutafuta suluhisho.
Amaar alielezea matarajio makubwa kwa mkutano huo wa
Beijing, akitumaini kuwa utaweka ajenda mpya ya kimataifa ya kukuza haki za
wanawake, sawa na Azimio la Beijing na Jukwaa la Utekelezaji lililopitishwa
mwaka 1995.
“Miaka thelathini imepita tangu Azimio la Beijing na Jukwaa
la Utekelezaji yalipoweka msingi wa juhudi za kimataifa za kisheria za
kuimarisha na kulinda haki za wanawake,” alisema.
Aliongeza kuwa mkutano huu unafanyika katika kipindi ambacho
dunia inapitia mageuzi makubwa ya kiuchumi, kisiasa, kidijitali na
kiteknolojia.
Amaar alisisitiza kuwa Azimio la Beijing na Jukwaa la
Utekelezaji vimekuwa ramani ya njia inayoziongoza nchi katika juhudi zao za
kuwawezesha wanawake.
Akionyesha uhusiano thabiti kati ya Misri na China, Amaar
alibainisha kuwa ushirikiano wa pande mbili umechangia maendeleo makubwa katika
sekta ya elimu ya kiufundi na ufundi stadi nchini Misri.
Alisema kuwa programu za mafunzo ya ufundi zinazotolewa na
China kwa wanawake zimewasaidia kuboresha ujuzi wao wa kitaaluma, kuongeza
nafasi za ajira na kuimarisha uhuru wa kifedha kwa kuwaandaa vyema zaidi kwa
soko la ajira.
Amaar pia alisifu maendeleo ya kiuchumi ya China, akisema
yamewanufaisha wanawake kwa kiasi kikubwa.
“China imevunja dhana potofu za elimu kwa kufungua shule za
ufundi katika nyanja kama vile kilimo, ujenzi na biashara mtandaoni, ili
kuwawezesha wanawake kiuchumi,” aliongeza.
Amaar alisisitiza kuwa Misri kwa sasa inashuhudia “enzi ya
dhahabu” kwa wanawake, ikitegemea Katiba ya mwaka 2014 ambayo imeweka mfumo
imara wa kisheria na kikatiba wa kulinda haki na mafanikio ya wanawake.
Alitaja maendeleo yaliyopatikana katika sekta mbalimbali,
hasa ushiriki wa kisiasa.
“Misri imepiga hatua
kubwa katika kuwawezesha wanawake kisiasa, ikifikia uwakilishi usio na kifani
wa asilimia 27 katika Bunge na asilimia 14 katika Seneti,” alisema.
Aliongeza kuwa Bunge la sasa limepitisha sheria kadhaa za
kulinda haki za wanawake, ikiwemo hatua za kuzuia ukeketaji, kupambana na
unyanyasaji wa kijinsia na kulinda haki za urithi.
Kuhusu uwezeshaji wa kiuchumi, Amaar alisisitiza maendeleo
makubwa ya Misri katika kuwaunganisha wanawake katika biashara ndogo na za
kati, na kuwaandaa kuingia kwenye soko rasmi la ajira.
Alitaja mpango wa “Tahwisha”, ambao ni mpango wa kidijitali
wa kuweka akiba na kukopa, unaowawezesha wanawake walioko maeneo ya vijijini
kufungua akaunti za benki, kuweka akiba na kupata mikopo ya kuanzisha biashara
ndogo.
“Mpango huu umechangia pakubwa katika kuwawezesha wanawake
wa Misri kiuchumi,” alisema.
Amaar pia alionesha kuthamini kwake Mpango wa Utawala wa
Ulimwengu (Global Governance Initiative), akisema kwamba “katika dunia yenye
haki, wanawake ndio wa kwanza kunufaika,” kwa kuwa mara nyingi wao ndio
huathiriwa zaidi na migogoro, mizozo na misukosuko ya kiuchumi.
“Ikiwa tutaishi katika dunia yenye haki zaidi inayotetea
maadili ya kweli na kukataa viwango vya ubaguzi, tutaweza kufikia amani ya
dunia — jambo ambalo hatimaye litawanufaisha wanawake,” aliongeza.









© Radio Jambo 2024. All rights reserved