
Aliyekuwa Waziri wa Utumishi wa Umma, Justin Muturi, ameweka
wazi sababu za kutohudhuria vikao vya Baraza la Mawaziri, akisisitiza kuwa
ilikuwa hatua ya kimaadili na si uzembe wa majukumu.
Akizungumza Jumatano katika mkutano na wanahabari katika jumba la Ufungamano, Muturi alisema kuwa suala la utekaji na mauaji ya kiholela liliendelea kupuuzwa katika mijadala ya Baraza la Mawaziri, hali iliyomsukuma kususia vikao hivyo.
Alifichua kuwa hakuhudhuria makusudi vikao vitatu vya Baraza la Mawaziri vilivyofanyika mapema mwaka huu, kuanzia kikao cha kwanza Januari 21 katika Ikulu Ndogo ya Kakamega.
“Nilipopokea mwaliko na ajenda ya kikao hicho, niligundua kuwa suala la utekaji na mauaji ya kiholela halikujumuishwa,” Muturi alieleza.
“Sikuona inafaa kushiriki kikao kinachopuuzilia mbali suala nyeti kama hili, ambalo ni msingi wa katiba yetu na utawala wa sheria.”
Muturi alisema alituma rasmi barua kwa Rais William Ruto kupitia Katibu wa Baraza la Mawaziri mnamo Januari 20, 2025, akijieleza kwa nini hatohudhuria na kusisitiza haja ya mjadala wa dharura kuhusu madai ya ukiukaji wa haki za binadamu.
Hata hivyo, licha ya kuibua suala hilo, kikao cha pili cha Baraza la Mawaziri mnamo Februari 11, 2025, kilikiuka mjadala huo tena.
“Nilikagua ajenda na nikagundua kuwa suala hilo bado halikuwa limeorodheshwa,” Muturi alisema.
“Kisha nikamwandikia Rais moja kwa moja, nikimwomba alipe kipaumbele kwa ajili ya mjadala na uamuzi.”
Alisema hali hiyo iliendelea hata katika kikao cha tatu cha Baraza la Mawaziri mnamo Machi 11, 2025.
“Mara nyingine tena, suala hilo halikujumuishwa kwenye ajenda,” alisema.
“Niliandika barua nyingine kwa Rais, nikimkumbusha msimamo wangu na kumhimiza kutilia maanani suala hilo.”
Muturi alisema hakupokea majibu yoyote kwa barua zake zote, hali iliyomfanya aamini kuwa Rais hakutilia maanani suala hilo.
Aidha, alielezea mshangao wake baada ya Rais Ruto kusema hadharani kuwa Baraza la Mawaziri lilikuwa limeshajadili na kutatua suala hilo.
“Nilishtushwa kumsikia Rais moja kwa moja kwenye televisheni akidai kuwa suala hilo limeshajadiliwa na kutatuliwa,” Muturi alisema.
Pia alihoji msimamo wa Rais kuhusu madai ya kuvunjwa kwa kikosi cha polisi kinachodaiwa kuhusika na utekaji na mauaji.
“Iwapo Rais alifahamu kuwepo kwa kikosi kama hicho, ambacho kilihusika na uhalifu huo wa kutisha, mbona washukiwa wake hawajakabiliwa na mkono wa sheria?” aliuliza.
“Kwanini Rais hajawataja wahusika ili wafikishwe mahakamani kwa uhalifu waliotenda?”
Muturi pia alieleza hofu yake kuhusu utekaji unaoendelea, akitaka ufafanuzi iwapo kikosi kingine kimeundwa kuchukua nafasi ya kile kilichodaiwa kuvunjwa.
Alisisitiza kuwa kufutwa kwake kazi kulihusiana moja kwa moja na msimamo wake thabiti kuhusu suala hilo, na wala si kwa sababu ya kutohudhuria vikao vya Baraza la Mawaziri.
“Nitaendelea kupigania haki na uwajibikaji, bila kujali gharama ya kibinafsi,” alitangaza.
Muturi alieleza kuwa alianzisha kampeni dhidi ya utekaji mnamo Januari 12, 2025, baada ya kufichua kuwa mwanawe alikuwa mwathiriwa.
Baadaye alieleza kuwa mwanawe aliachiliwa huru kufuatia
uingiliaji kati wa Rais.