
Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Falhada Dekow Iman, ameomba msamaha hadharani kufuatia vurugu zilizotokea katika viunga vya Bunge la Kitaifa siku ya Jumanne, ambapo alinaswa kwenye video akizozana na Mbunge wa kuteuliwa wa ODM, Umulkheir Harun..
Tukio hilo, lililonaswa moja kwa moja na kamera na kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii, lilizua hisia kali miongoni mwa wananchi. Wawili hao walionekana wakitupiana maneno ya matusi kabla ya kushikana, huku baadhi ya wabunge wenzao wa kike wakijaribu kwa juhudi kubwa kuwatuliza – bila mafanikio. Afisa wa usalama wa Bunge aliingilia kati na kuwatawanya, lakini hali ya taharuki iliendelea hata baada ya wawili hao kutenganishwa.
Akizungumzia tukio hilo kwa mara ya kwanza, Falhada alitoa taarifa rasmi akieleza masikitiko yake na kuchukua jukumu kamili kwa matendo yake.
“Yaliyotokea ni kinyume kabisa na maadili ya taasisi tunayoihudumia na imani ya wananchi waliotupa dhamana ya kuwaongoza. Kwa hili, naomba radhi kwa dhati,” alisema, akisisitiza kuwa tukio hilo halipaswi kurudiwa.
Mwanasiasa huyo alieleza kuwa ugomvi huo ulitokana na msururu wa maneno ya uchokozi kutoka kwa mwenzake, na licha ya kujaribu kuvumilia, alijikuta akishindwa kujizuia kutokana na mazingira ya kikao kilichokuwa na mvutano mkubwa.
“Katika hasira, nilivuka mipaka ya uongozi wa kiungwana. Hakuna hali inayoweza kuhalalisha tabia hiyo, nami ninachukua jukumu kamili,” aliongeza.
Falhada alisisitiza kuwa tofauti za kisiasa hazipaswi kushughulikiwa kwa njia ya mabishano au fujo, bali kupitia mazungumzo na nidhamu.
Pia alieleza kuwa amejitafakari na atatumia tukio hilo kama funzo la kuboresha utendaji wake kama kiongozi.
“Nitajifunza kutokana na hili, na ninajitolea tena kuzingatia
maadili, heshima na taaluma ya uongozi,” alisema.
Kwa upande wake, Umulkheir Harun alitoa tamko la awali muda mfupi baada ya tukio, akilaani fujo hiyo na kusema amepeleka malalamiko rasmi kwa taasisi husika.
“Ninajutia sana tukio hili, na nataka kusisitiza kuwa siungi mkono aina yoyote ya tabia isiyo ya nidhamu,” alisema, huku akiitaka jamii ya kisiasa kuendeleza mazingira ya kuheshimiana.
Hadi sasa, haijabainika wazi chanzo kamili cha ugomvi huo, wala hatua rasmi zitakazochukuliwa na uongozi wa Bunge.
Hata hivyo, tamko la wawili hao linaashiria hatua ya kujenga
upya maadili na ustaarabu katika ulingo wa siasa.