Polisi katika eneo la Kisumu Mashariki wameanzisha msako mkali kumtafuta mwanamume anayedaiwa kumvamia mpenzi wake wa zamani na kumjeruhi vibaya kwa madai ya kuachwa kwa ajili ya mwanamume mwingine.
Kulingana na taarifa ya DCI, mshukiwa huyo anayefahamika kama Sebi Obonyo alimuandama mpenzi wake wa zamani, mwenye umri wa miaka 24, hadi katika nyumba ya mpenzi wake mpya katika kijiji cha Nyakbong', eneo la Kamjulu, Kisumu Mashariki, siku ya Ijumaa majira ya saa kumi na moja kasorobo jioni.
Katika tukio hilo la kutisha, Obonyo anadaiwa kumchoma mpenzi wake mara mbili kwa kutumia kitu chenye ncha kali — sikio la kushoto na sehemu ya kifua — kabla ya kutoroka, kwa mujibu wa DCI.
“Mshukiwa alimuandama hadi alipokuwa akiishi na mpenzi wake wa sasa, kisha akamchoma kifuani na sikioni kwa kutumia silaha kali, kabla ya kutoroka eneo la tukio,” ilisema DCI kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii.
Kilio cha mwathiriwa kilivutia majirani waliokimbia kumsaidia, hali iliyomlazimu mshukiwa kuhepa kabla ya kuhakikisha hali ya majeruhi wake.
“Kwa bahati nzuri, majirani walifika kwa wakati na kumuokoa, lakini alikuwa akivuja damu kupita kiasi,” ilieleza taarifa hiyo ya DCI.
Msichana huyo alipelekwa kwa haraka katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Jaramogi Oginga Odinga ambapo bado amelazwa katika hali mahututi huku madaktari wakifanya juhudi za kuokoa maisha yake.
DCI imewataka wananchi kushirikiana na maafisa wa usalama ili kusaidia katika kukamatwa kwa mshukiwa huyo ambaye bado yuko mafichoni.
“Tunatoa wito kwa yeyote mwenye taarifa kuhusu mshukiwa huyu kuwasiliana nasi au kuripoti katika kituo cha polisi kilicho karibu,” DCI ilihitimisha.