logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Ushauri mzito wa aliyekuwa naibu gavana Vihiga kwa viongozi baada ya kujikuta akiuza kuni ili kujikimu

Amaswache sasa huonekana akitembea mitaani na mafungu ya kuni, akiwauzia wateja wake hasa wamiliki wa hoteli ndogo ndogo.

image
na Samuel Mainajournalist

Yanayojiri19 April 2025 - 10:27

Muhtasari


  •  Amaswache alielezea masaibu anayopitia tangu aondoke ofisini, akifichua kuwa hawezi tena kugharamia mahitaji ya familia yake, ikiwemo ada ya shule ya binti yake.
  • Sasa, anatoa wito kwa Rais William Ruto na serikali kwa ujumla kuwajali waliowahi kuhudumu serikalini lakini sasa wanaishi kwa mashaka.

Aliyekuwa naibu gavana wa Vihiga Caleb Amaswache sasa anauza kuni ili kujikimu

Aliyekuwa Naibu Gavana wa Kaunti ya Vihiga, Caleb Amaswache, ametoa wito wa kutafakarisha viongozi walioko mamlakani, baada ya maisha kubadilika ghafla na kumlazimu kujitafutia riziki kwa kuuza kuni mitaani mjini Luanda.

Amaswache, ambaye alihudumu kati ya mwaka 2013 hadi 2017 chini ya utawala wa Gavana wa zamani Moses Akaranga, sasa huonekana akitembea mitaani na mafungu ya kuni, akiwauzia wateja wake hasa wamiliki wa hoteli ndogo ndogo.

Hali yake ya sasa inakinzana pakubwa na maisha ya kifahari aliyokuwa akiishi akiwa serikalini, ambapo alikuwa na mshahara wa zaidi ya shilingi laki sita kwa mwezi, magari ya kifahari na ulinzi mkali.

Katika mahojiano ya hivi majuzi na runinga ya Citizen, Amaswache alielezea masaibu anayopitia tangu aondoke ofisini, akifichua kuwa hawezi tena kugharamia mahitaji ya familia yake, ikiwemo ada ya shule ya binti yake.

“Mtaji sina. Nina binti anasoma na ninahitaji angalau shilingi laki mbili kuanzisha biashara vizuri. Wakati mwingine napata mia mbili tu kwa siku,” alisema kwa masikitiko.

Amaswache alifichua kuwa licha ya kuwasilisha maombi ya kazi katika nafasi tofauti serikalini, juhudi zake hazijazaa matunda. Alitaja kutoitwa kwenye usaili wa nafasi za makamishna wa IEBC kama mfano wa kukataliwa kwake.

Sasa, anatoa wito kwa Rais William Ruto na serikali kwa ujumla kuwajali waliowahi kuhudumu serikalini lakini sasa wanaishi kwa mashaka.

Naomba kazi. Mheshimiwa Rais, tafadhali tuangazie waliowahi kuwa serikalini. Sisi sote ni Wakenya. Tusisahauliwe mara tu tukitoka madarakani,” aliomba kwa unyenyekevu.

Katika ujumbe wake kwa viongozi waliopo mamlakani, Amaswache anawahimiza kuwa na heshima kwa waliowatangulia na kutambua kuwa mamlaka si ya kudumu.

“Mnapokuwa madarakani mnaheshimiwa, mnaonekana. Lakini mnapotoka, wengi hawapokei hata simu zenu. Hapo ndipo mtu anafahamu maana halisi ya maisha,” alisema kwa uchungu.

Wakazi wa Luanda wanaonunua kuni kutoka kwake pia wameungana naye kumwombea msaada, wakisema mtu wa hadhi yake hastahili kuishi katika hali ya unyonge namna hiyo.

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved