
Wawakilishi wadi hao wakizungumza kwenye vikao na wanahabari wametaja maneno ya gavana huyo kama propaganda ambazo hazina ukweli. Wameendelea na kuilaumu serikali ya kaaunti hiyo kwa kuondoa kwenye bajeti fedha za kulipia madeni ya awali.
"Juzi kama wiki mbili zilizopita, tulishikwa na mshangao. Wananchi walipigwa na butwaa kufatia matamshi ya mheshimiwa gavana wetu. Ambaye alisema ya kwamba MCAs wa Busia wanapewa shilingi milioni 20 ili kufanya miradi katika wadi zao. Nataka kuelezea wananchi kwamba tukiangalia katika mipangilio ya bajeti, Mwaka wa kwanza tukiingia pale bungeni, Mwaka wa fedha 2022/2023 wadi zilipewa shilingi milioni 8 pekee ya kufanya miradi. Mwaka 2023/2024 wadi zilipewa milioni 11 za kufanya kazi," alisema Bonventure Makoha wa wadi ya Buhayo ya kati.
"Ukweli ni kwamba wakati huu sisi kama MCAs tunapitia mambo magumu sana kwa wadi zetu, kwa sababu wananchi wetu wanaamini kwamba MCAs wamepatiwa pewsa na wako nazo kwa mfuko. Imetuletea shinda na tumekuwa na wakati mgumu sana kujieleza kwa wananchi. Sisi hatupokei pesa gavana ndiye anayefanya kazi kwa wadi zetu," aliendelea kueleza.
"Gavana wetu Otuoma alisema kwamba anaenda kumalizana na pending bills. Lakini kuanzia mwaka wa kwanza, pili mpaka leo hakuna fedha zozote zilizotengwa kwa ajili ya madeni," walieleza zaidi.
Wakati huohuo wamemtaka gavana Otuoma kujitokeza wazi na kurekebisha matamshi yake mbele ya umma kwani yameharibu pakubwa uhusiano wao na wananchi. Wakati huo baadhi ya waakilishi wadi hao wameapa kutopitisha bajeti ya ziada ya mwaka 2025/2026.
Gavana Otuoma awali alikuwa amesema kwamba alitoa fedha zaidi ya milioni 20 kwa kila wadi na kuwataka wawe tayari kueleza miradi yao kwa wananchi.
"Kwa mfano hiyo pesa uchukue kama hapa Samia kama ziko wadi nne, tayari hiyo ni milioni 80, pamoja na zile tunaongeza ni zaidi ya shilingi milioni 100. Pesa ambazo zinatoshana na za mgao wa Usitawi wa maeneobunge CDF. Sasa badala wewe useme umefanya nini kwa wadi yako, mbunge akisema amefanya nini na wewe pia unasema umefanya nini, " alieleza Otuoma.
Vile vile akizungumza aliwataka wawakilishi wadi kuwa tayari kubeba misalaba yao siku ya kiama itakapofika iwapo watashindwa kueelezea wenyeji kile ambacho watakuwa wamekifanya kwa miaka mitano.
"Kila mtu kwa wodi yake atahesabu kazi yake wala sio kulaumu gavana, siku ya kiama ikifika kila mtu atajitetea. Kwa sababu nimepeana bilioni mia saba kwa wawakilishi wadi wote kwa pamoja na hizo ni pesa nyingi sana. Hakuna sheria ambayo inasema nafaa kuwapatia hiyo pesa. Mlifanya kampeni mkiahidi na tumewapea mtimize," aliweka wazi Otuoma.