
GEORGINA Njenga amevunja kimya chake kuhusu kuvunjika kwa uhusiano wake na aliyekuwa mpenzi wake, Tyler Mbaya maarufu Baha Machachari.
Akizungumza kwenye podkasti ya Morin Actress, Njenga
alifichua kwamba ifikapo Mei mwaka huu, watamaliza miaka 2 tangu kuachana kwao.
Mama huyo wa binti mmoja alipoulizwa kuhusu chanzo cha
kusambaratika kwa huba lao na kumweka binti yao njia panda kukosa penzi la
mzazi mmoja kati yao, alisema kwamba baada ya kutathmini kwa muda, wakati
mwingine anahisi haikufaa kuwa sababu kubwa ya kusababisha kuachana kwao.
Georgina Njenga alikiri kwamba kuna wakati huwa anakaa chini
ya kujuta kuvunja uhusiano wake na baba wa mwanawe, akitania kwamba mitaani
kuna baridi sana.
“Tuliachana miaka miwili
iliyopita, inaelekea miaka 2 ikifika Mei. Kilichoniuma zaidi ni kuvunjika kwa
familia, ikilinganishwa na kuvunjika kwa penzi,” alisema.
“Hata haikuwa sababu ya
msingi sana, nilikuja kuifikiria (baadae) ni kama ilikuwa ya msingi kidogo
lakini kwa sasa kusema ukweli kuna wakati mwingine mimi hujuta kuondoka. Kwa sababu
mitaani kuna baridi. Lakini majuto ni kama 2%,” Njenga aliongeza.
Kuhusu kilichomuuma zaidi katika harakati ya kutengana kwake
na Tyler Mbaya, Georgina Njenga alisema kwamba aliumia zaidi kuona familia
ikisambaratika kuliko kuona penzi likimwagika.
“Nilikuwa nakaa tu hivi
najiambia kwamba nilikua bila baba na hapa binti yangu nitamuona akikua bila
baba… lakini pia nilikuwa najijibu kwamba siwezi teseka kwa sababu ya mtu
(mtoto) ambaye atakua na aondoke kuishi maisha yake aniwache,” Njenga alisema.
Hata hivyo, alisema kuwa majuto hayo yanakuja kwake kwa njia
nyepesi kwani huwa anafikiria kwamba akitathmini jinsi alivyoondoka, pengine
angepewa nafasi ya kufanya maamuzi upya angeshughulikia suala hilo kwa njia
tofauti.
Ingawa uhusiano wao haukufanikiwa, Georgina alikiri kwamba
uzazi wa ushirikiano umeboreka baada ya muda.
Alimsifu mama yake kwa kuchukua jukumu muhimu katika kumlea
binti yao na kuwezesha mawasiliano kati yake na Baha.
Akieleza kwamba kwa vile Baha mara nyingi huzungumza na mama
yake, kuna haja ndogo ya mawasiliano ya moja kwa moja kati yao.
Georgina na Baha walikuwa mmoja wa wanandoa wachanga
waliopendwa sana nchini Kenya, lakini walitengana mwaka wa 2023, miezi michache
tu baada ya kumkaribisha binti yao.