

FAMILIA ya Esther Musila imetupwa kwenye kipindi cha maombolezo baada ya kufiwa na kijana ambaye amekuwa akimlea kama mwanawe.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Musila
alisimulia kwa uchungu jinsi kifo kimeipokonya familia mtu wa maana ambaye
alikuwa na asilimia kubwa ya maisha yake mbele yake.
Musila alifichua kwamba kijana huyo ambaye
alikuwa ndio anajiandaa kujiunga na chuo kikuu amefariki, takribani miaka saba baada ya kuwazika wazazi wake wote.
“Kwa mwana ambaye nilimpenda kama wangu,
hili limeniuma sana. Ni takribani mwaka mmoja tangu tuwazike wazazi wako,
nilizungumza na wewe siku mbili zilizopita na Nilifurahia mipango yako ya
kujiunga chuo kikuu na nilitegemea kukuona ukitimiza ndoto zako za kuwa
mwanasayansi,” Musila aliomboleza.
Musila alikumbuka jinsi kijana huyo na mwanawe
Glenn Naibei walikulia Pamoja kama kaka na dada wa tumbo moja tangu darasa la
kwanza.
Musila alisema kwamba kando na kuhisi kupata
pigo, amekasirika kwamba kijana huyo amefariki angali na umri mbichi kabisa
kama jani la mgomba.
“Hukustahili kufa kwa jinsi hii, nina
hasira. Baadhi yetu tulikufeli. Pumzika kwa amani mwanangu kwa maana sasa
umeungana na wazazi wako ambao walikulea kwa nguvu zote wakati wa siku zao za
mwisho duniani. Naamini walikuona ukitaabika na walikutaka uungane nao. Pumzika
vizuri Malakwen,” Musila alimaliza.
Hata hivyo, hakuweka wazi kiini cha kifo cha
kijana huyo licha ya kudokeza kwamba watu wake wa karibu, akiwemo yeye huenda
walimfeli kwa njia Fulani kupelekea kifo chake.