Asubuhi tuliyojaa utulivu, ndani ya darasa lililofunikwa na mwanga wa jua katika Taasisi ya Confucius katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kundi la walimu wa Kichina waliendelea kurudia salamu za Kiswahili.
“Habari za asubuhi,” alisema mmoja
kwa tabasamu.
“Nzuri sana,” alijibu mwingine.
Ubadilishanaji huu rahisi, “habari za asubuhi” na “nzuri sana”, ni zaidi ya somo la lugha. Unawakilisha harakati inayokua ya udadisi wa kitamaduni, heshima ya pande zote mbili, na kubadilishana elimu kati ya China na Tanzania.
Wakati jumuiya ya kimataifa ilipotambua Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani Jumatatu, roho ya siku hiyo ilionekana wazi katika Taasisi ya Confucius ya chuo kikuu kikubwa zaidi nchini Tanzania, ambapo raia wa Kichina walikuwa wakikumbatia Kiswahili si tu kama lugha bali kama mlango wa kuelewa maisha ya hapa.
Kiswahili, pia kinachojulikana kama lugha ya Swahili, ni moja ya lugha zinazozungumzwa sana barani Afrika, likitumika kama lugha ya mawasiliano katika Afrika Mashariki na Kati.
Mkutano mkuu wa UNESCO, katika kikao cha 41 kilichofanyika mjini Paris, Ufaransa, mwaka 2021, ulitangaza Julai 7, kila mwaka Siku ya Lugha ya Kiswahili duniani - na hivyo kuwa lugha ya kwanza ya kiAfrika kutambuliwa hivyo na Umoja wa Mataifa.
Yang Xin, mwalimu wa lugha ya Kichina katika Taasisi ya Confucius, alisema kujifunza Kiswahili imekuwa changamoto na pia ni hitaji.
“Mwanzoni, sikuweza kuelewa
chochote,” alikumbuka.
“Lakini kwa msaada wa Taasisi ya Confucius, nilianza kujifunza. Inanisaidia
kuzoea maisha hapa na kuwasiliana na watu.”
Zou Zhenzhen, mwalimu mwingine wa Kichina, alisema:
“Hata kutumia maneno machache tu ya Kiswahili darasani huleta tofauti. Inaonyesha wanafunzi kuwa tunaheshimu utamaduni wao, na inawafanya wawe na hamasa zaidi ya kujifunza Kichina. Unaweza kuuona uso wao unavyobadilika.”
Mbinu yao ni rahisi lakini yenye
ufanisi: kuomba msaada, kufanya mazoezi nje ya darasa, na kutumia kile
ulichojifunza wakati wa kununua chakula, kuchukua teksi, au kuzungumza na
marafiki.
Zou aliongeza:
“Sasa naweza kuagiza chakula, kuzungumza na dereva wa teksi, na hata kufanya masihara na marafiki. Lugha huvunja barafu.”
Walimu wote wa Kichina wamekuwa wakijifunza Kiswahili kwa miezi miwili iliyopita, wakihudhuria vipindi viwili vya masaa mawili kila Jumapili.
Athari ya kuelewa Kiswahili zaidi ya darasani inaenea
Kwa mujibu wa Emmanuel Legonga, mwalimu wa lugha wa Kitanzania anayefundisha Kiswahili na Kichina katika Taasisi ya Confucius na pia huwafundisha raia wa Kichina nchini Tanzania, kuzungumza lugha ya hapa kunaleta athari ya moja kwa moja katika sekta mbalimbali.
“Katika miradi ya miundombinu kama
reli na bandari, pale wasimamizi au wahandisi wa Kichina wanapotumia Kiswahili,
hujenga imani na wafanyakazi wa hapa,” alieleza Legonga.
“Huondoa hisia ya umbali. Wafanyakazi hujihisi kuonekana, kuheshimiwa.”
Hii ni muhimu hasa katika miradi ya Sera ya Ukanda na Njia (BRI), ambapo ushirikiano mkubwa kati ya wataalamu wa Kichina na Watanzania ni wa lazima.
“Lugha hufungua mlango wa uwazi. Hupunguza kutoelewana na hujenga kuaminiana,” aliongeza.
Legonga alifurahi kutaja kuwa mmoja wa wanafunzi wake wa Kiswahili ni Zhang Xiaozhen, mkurugenzi mwenza wa Kichina wa Taasisi ya Confucius katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Kwa mtazamo wa Zhang, hamasa ya kujifunza Kiswahili miongoni mwa Wachina inaongezeka.
“Katika kipindi chetu cha mwisho,
zaidi ya Wachina 70 walijiunga na madarasa ya Kiswahili. Mwaka huu, karibu 90
wamejiandikisha,” alisema Zhang.
“Wengine huanza kujifunza wakiwa China, wengine baada ya kufika hapa. Takribani
walimu 20 wa Kichina wameshasoma Kiswahili.”
Zhang mwenyewe hujifunza Kiswahili kadri ratiba yake inavyoruhusu.
“Lugha ni daraja. Huunganisha watu. Na Kiswahili kinazidi kuwa muhimu — si tu Afrika Mashariki bali hata kimataifa,” alisema.
Zhang aliona pia mfanano wa
kitamaduni kati ya Tanzania na China.
“Dhana
ya Ujamaa ya Tanzania, ushirikiano na jamii inalingana na thamani za pamoja za
China. Katika tamaduni zote mbili, familia na maelewano ni vitu vya msingi,”
alisema.
Mussa Hans, mkurugenzi mwenza wa Taasisi ya Confucius katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, anaulizwa maswali Dar es Salaam, Tanzania, Julai 4, 2025. (Xinhua/Emmanuel Herman)
Mussa Hans, mkurugenzi mwenza wa Taasisi ya
Confucius upande wa Tanzania, alipokuwa akijiandaa kusherehekea Siku ya Lugha
ya Kiswahili Duniani, alitafakari dhamira pana ya taasisi hiyo:
“Hatufundishi tu lugha; tunajenga mahusiano,” alisema.
“Tunakuza lugha ya Kichina na Kiswahili ili watu wetu waelewane vyema.”
Dira yao ni siku za baadaye ambapo mkurugenzi mwenza wa Kichina anazungumza Kiswahili kwa ufasaha, na mkurugenzi mwenza wa Tanzania anazungumza Kichina.
“Hapapaswi kuwe na kikwazo cha lugha
kati ya nchi zetu,” alisema Hans.
“Iwe unakwenda kutoka China hadi Tanzania au kinyume chake — jifunze Kiswahili,
jifunze Kichina.”