
Wasiwasi mkubwa umeibuliwa kuhusu hali ya
uhusiano wa mtangazaji wa runinga Betty Kyallo na mpenzi wake, Charles Kamau
Githinji, mwenye umri wa miaka 26.
Hii ni baada ya wawili hao, ambao kwa zaidi ya mwaka mmoja wamekuwa wakionyesha mapenzi yao hadharani, kuamua kuacha kufuatiliana kwenye mitandao ya kijamii. Awali, walikuwa wakifuatana kwenye akaunti zao kubwa za Instagram na mara kwa mara walichapisha picha na video wakiwa pamoja. Hata hivyo, hatua yao ya hivi karibuni imeacha wengi wakijiuliza iwapo uhusiano wao uko shakani.
Hali imezidi kuzua gumzo baada ya Charlie, ambaye ni mtaalamu wa teknolojia, kuchapisha jumbe tata kwenye Instagram yake, akiashiria kuwa huenda wameachana. Katika chapisho moja, alidokeza kuwa ana majuto aliyokuwa anataka kuyafichua:
"Kuna majuto mengi ambayo nipo karibu kuyaweka wazi?" aliandika.
Katika chapisho linguine siku ya Alhamisi asubuhi, alionekana kuthibitisha kuwa uhusiano wao wa zaidi ya mwaka mmoja umefikia kikomo, lakini akasisitiza kuwa hatamdhalilisha mpenzi wake.
"Ndio, tumeachana. Hata akiniaibisha, sitadanganya kuhusu jina lake. Aseme anavyotaka," aliandika.
Akaongeza: "Usiseme uongo kunihusu, nami sitasema ukweli kukuhusu."
Charlie pia alipakia meme ikionyesha kuwa anajitambua kwamba yeye sio mzuri kabisa na hajali jinsi anavyochukuliwa na watu.
Katika chapisho lingine,
alizungumzia afya ya akili ya wanaume, akieleza kuwa mara nyingi haizingatiwi
hadi mambo yanapozidi kuwa mabaya.
"Hakuna anayejali afya ya akili ya mwanaume hadi hasira itokee, ndipo kila mtu anaanza kumwona kama mtu mbaya," ilisomeka meme hiyo.
Haya yanajiri siku chache tu baada ya Betty na Charlie kuonekana pamoja hadharani kwa mara ya mwisho kwenye hafla iliyoandaliwa na msanii Bahati na mkewe Diana Marua kusherehekea uhusiano wao.
Wakati wa hafla hiyo mwanzoni mwa
mwezi huu, Charlie alimsifia Betty hadharani na kuweka wazi kuwa anampenda
sana. Betty pia alionekana kufurahia sana kuwa na mpenzi wake, huku wawili hao
wakishiriki nyakati tamu za kimapenzi.
Hata hivyo, baada ya matukio haya ya hivi majuzi, wengi wanajiuliza—je, penzi lao limefika mwisho bila kutarajiwa?