Machozi ya furaha yalimtiririka mjane wa marehemu Charles Bukeko almaarufu kama Papa Shirandula baada ya mtangazaji Jalang'o kutangaza kuwa angechukua jukumu la kuelimisha binti yake mdogo kwa jina Sherry.
Wakiwa kwenye hafla ya kuadhimisha mwaka moja tangu kuaga kwa mwigizaji na mcheshi tajika Papa Shirandula ambayo ilifanyika Jumapili, Jalang'o aliahidi kuwa angegharamia karo yote ya Sherry hadi chuo kikuu kwa ushirikiano na wacheshi wenzake Captain Otoyo na Njoro.
"Sisi watatu; Jala, Otoyo na Njoro tunataka kuchukua jukumu la kulipa karo yote ya binti yangu hapa (Sherry). Kutoka leo mama usiwahi jali tena mambo ya karo. Tungetaka utuletee taarifa ya karo iwe leo, iwe kesho mimi mwenyewe nitakupatia cheki ya kutoka saa hii hadi amalize shule ya msingi na hata akiingia kidato cha kwanza mambo yake usiwahi jali. Kutokea leo Sherry ni wetu": Jalang'o alitangaza.
Mtangazaji huyo alisema kuwa alimtaka marehemu Papa afurahi kutoka mahali aliko kwani isingalikuwa ni yeye hawangekuwa hawangekuwa wamepata mafanikio ambayo wanayo kwa sasa.
Mjane wa Papa ambaye alikuwa amewezwa na hisia aliwashukuru kwa kitendo chao cha ukarimu.
"Nashukuru Mungu kwani yeye ni Mungu wa suluhu. Kile ambacho Jalang'o amefanya kimeyeyusha moyo wangu. Ni wiki moja tu niliwanga nafikiria kuhusu karo ya shule. Mungu ameleta suluhu. Asante." Mkewe Bukeko alisema
Watatu hao walijitolea kusaidia binti ya mtu ambaye aliwafungulia milango ya sanaa na kuwapa umaarufu mkubwa nchini kama ishara ya heshima.
Bukeko aliaga mnamo Julai 18 alipokuwa anakimbizwa hospitali kutokana na matatizo ya kupumua.