
MAKACHERO wa upelelezi wa jinai, DCI wametoa taarifa kuhusiano na ripoti za kuwepo kwa raia wa kigeni wanaoshirikiana na wakenya kufungua maabara ya kutengeneza dawa za kulevya katika mji wa Namanga kaunti ya Kajiado.
Taarifa ya DCI ilijiri saa chache baada ya jarida moja la
humu nchini kuchapisha simulizi kuhusu maabara hiyo ya kutengeneza dawa za
kulevya iliyohusishwa na raia wa Mexico, Nigeria na Kenya.
Katika taarifa yao, DCI walikiri kwamba kulikuwepo na watu
hao lakini msako wao mwezi Septemba mwaka jana ulifanikisha kukamatwa kwa
baadhi yao ambao kesi inaendelea katika mahakama ndogo ya uwanja wa ndege,
JKIA.
“Baada ya kuanzisha
uchunguzi, mshukiwa wa kwanza (Mkenya) alikamatwa mnamo Septemba 16, 2024
katika nyumba yake Ruiru. Anaaminika kuongoza ujenzi wa maabara hiyo haramu kwa
ushirikiano na mshukiwa wa pili (Mnigeria),” DCI walifichua.
Pia katika nyumba yake, walipata bidhaa kadhaa zikiwemo
kemikali za kutengeneza dawa na idhibati za kununua shamba hilo la Namanga.
Uchunguzi wa kina ulibaini uhusiano kati ya Mkenya huyo na
raia wawili wa Nigeria ambao pia walibainika kuwa na mawasiliano na raia wa
Mexico ambaye aliwahi kuwa polisi nchini mwao.
“Uchunguzi pia
ulituelekeza kwa mshukiwa wa 4, raia wa Mexico – afisa wa zamani wa kitengo cha
upelelezi cha Mexico, alikamatwa katika uwanja wa JKIA akiwa mbioni kutorokea
kwao.”
DCI ilibaini kwamba raia huyo wa Mexico ni miongoni mwa
wengine wawili kutoka taifa hilo ambao waliletwa nchini Kenya na mshukiwa
kutoka Nigeria.
Idara hiyo ilibaini kwamba upelelezi wao umebaini kwamba
biashara ya kimataifa ya dawa za kulevya inayozungushwa kati ya mataifa ya
Nigeria, India, Mexico, Gabon na Afrika Kusini.