
RAIS William Ruto amefichua jinsi mpango wa bima ya kitaifa SHA unavyozidi kupata uungaji mkono na Imani kuu kutoka kwa Wakenya.
Akizungumza na Wakenya wanaoishi nchini China, rais Alifichua
kwamba SHA inazidi kuboreka kila siku huku akifichua kwamba huwa anapokea
taarifa za takwimu za SHA kila siku kutoka kwa mamlaka husika.
Kiongozi wa nchi alibainisha kwamba jana alipokea takwimu
zikionyesha kwamba jumla ya wakenya takribani elfu 55 walijiandikisha kwenye
SHA kwa siku hiyo pekee.
Rais alisema kwamba kwa kila siku, wastani wa Wakenya
wanaojisajili kwenye SHA ni kati ya 45,000 hadi 60,000, akipongeza Wakenya kwa
kuonyesha Imani yao kwa bima hiyo mpya.
“Tumenanzisha mpango wa
huduma ya afya kwa wote ambayo aghalabu inajulikana kama Taifa Care ama SHA. Na
nilikuwa naangalia kwa takwimu usiku wa jana, huwa napata ripoti kila siku
majira ya saa nne usiku.”
“Jana Wakenya 55,000
walijiandikisha kwa SHA. Kwa wastani, kila siku wakenya kati ya 45,000 na 60,000
hujiandikisha kwenye SHA,” rais alieleza.
Alisema kwamba SHA ni bima bora kwani inanufaisha kila mtu
hadi wale watu ambao hawajawahi kuwa chini ya bima yoyote ya afya katika maisha
yao.
“Kwa mara ya kwanza watu
ambao hawajawahi kuwa na bima yoyote ya afya sasa wanapata huduma ya bima ya
afya. Kwa miaka ya nyuma, NHIF ilikuwa imetengwa mahususi kwa watu ambao ama
wana mshahara au wenye walikuwa katika nafasi ya kulipia.”
“Lakini safari hii
tumeanzisha huduma ya afya kwa wote, jambo ambalo kwa muda mrefu tulikuwa
tunataka kufanya. Nakumbuka serikali ya NARC ilitaka kulifanya, na pia
nakumbuka tulijaribu kulifanya katika serikali ya Jubilee, na hatukuweza
kufanikiwa. Lakini najivunia kwamba safari hii tuliweza kufanikisha,” Ruto aliongeza.
Rais Alifichua kwamba
mpango wa kuzindua SHA ulichukua mchakato wa maandalizi kwa kipindi cha
takribani miaka 2.
“Tulichukua takribani
miaka 2 ya kupanga na kutengeneza mfumo sahihi na leo hii ninaweza sema kwa
ujasiri kwamba kinyume na NHIF ambayo ilikuwa na karibia watu milioni 7
waliojisajili, leo tuna watu milioni 21 waliojisajili kwenye SHA,” rais Ruto alikariri.