logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Wetang’ula Aonya Wakenya Dhidi ya Kuchochewa Kufanya Ghasia

Aliitaka sheria za maandamano ya umma kufanyiwa marekebisho ya haraka.

image
na Tony Mballa

Habari19 July 2025 - 09:56

Muhtasari


  • Aliwaagiza Kiongozi wa Wengi Bungeni Kimani Ichung’wah na wabunge kuongoza mchakato wa marekebisho ya sheria, miaka 15 baada ya Katiba ya 2010 kuanza kutumika, ili kufunga mianya inayoruhusu ghasia kujificha chini ya kivuli cha maandamano ya amani.
  • Kauli zake zinajiri huku mvutano wa kisiasa ukiongezeka kufuatia maandamano yenye ghasia ya Saba Saba, pamoja na ukosoaji mkali dhidi ya aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, ambaye Wetang’ula alimshutumu kwa “kusafirisha hulka mbaya za kisiasa” hadi Marekani.

Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula amewaonya Wakenya dhidi ya kuwaamini viongozi wanaowachochea kuingia kwenye ghasia.

Wetang’ula aliwakumbusha vijana kuwa viongozi wanaowachochea kuharibu mali na kuchoma vitu, mara nyingi huwa tayari na njia ya kutoroka nchi pindi mambo yanapoharibika.

“Wanasiasa na waandaaji wa maandamano wanapowahimiza vijana wetu wachome, wapore na waharibu huku watoto wao wakiendelea na masomo nje ya nchi, lazima wawajibishwe. Uhuru lazima uambatane na uwajibikaji,” alisema.

Aliitaka sheria za maandamano ya umma kufanyiwa marekebisho ya haraka.

Alionya kuwa haki ya kikatiba ya kuandamana imetumiwa vibaya mno, hali ambayo mara kwa mara husababisha ghasia, uharibifu wa mali na hata vifo.

Akizungumza wakati wa Mpango wa Kuwawezesha Wanawake Kiuchumi katika eneo la Kabuchoi, Wetang’ula alilaani wimbi la hivi majuzi la maandamano yenye vurugu, akisema kuwa hiyo ni kupotosha maana ya uhuru wa kikatiba.

“Tuambiane ukweli. Katiba inahakikisha haki ya kukusanyika na kuandamana, lakini haimpi mtu yeyote ruhusa ya kufanya ghasia, kupora, kuchoma mali, kubaka, kujeruhi au kuua,” alisema.

Moses Wetang'ula

“Hiyo ni utovu wa nidhamu, na hakuna jamii inayopaswa kuikubali.”

Akitoa mfano wa mfumo wa Uingereza, Wetang’ula alihimiza kuigwa kwa mfumo wa kisheria unaowawajibisha moja kwa moja waandaaji wa maandamano endapo ghasia au uharibifu utatokea.

“Tunapaswa kuiga mfano huu,” alisema.

Aliwaagiza Kiongozi wa Wengi Bungeni Kimani Ichung’wah na wabunge kuongoza mchakato wa marekebisho ya sheria, miaka 15 baada ya Katiba ya 2010 kuanza kutumika, ili kufunga mianya inayoruhusu ghasia kujificha chini ya kivuli cha maandamano ya amani.

Kauli zake zinajiri huku mvutano wa kisiasa ukiongezeka kufuatia maandamano yenye ghasia ya Saba Saba, pamoja na ukosoaji mkali dhidi ya aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, ambaye Wetang’ula alimshutumu kwa “kusafirisha hulka mbaya za kisiasa” hadi Marekani.

“Anachochea vurugu hapa nyumbani halafu anakimbilia Marekani kuigawanya diaspora,” alisema Wetang’ula.

“Watu anaowahutubia kule Marekani walizaliwa huko; hawajui makabila ya Kenya. Anasafirisha sumu ya siasa za Kenya hadi nje ya nchi.”

Aliongeza kuwa Gachagua hawezi tena kudai kuwakilisha mtu yeyote nchini Kenya na kuwataka wananchi kuwakatia tamaa viongozi wa aina hiyo.

“Huyo mtu hamwakilishi yeyote. Hata viongozi wa kawaida hawamheshimu. Lazima tudumishe amani, mshikamano na heshima ya pande zote,” alisema.

Wetang’ula aliandamana na viongozi wa Kenya Kwanza akiwemo Kiongozi wa Wengi Bungeni Kimani Ichung’wah, Kiranja wa Wengi katika Seneti Silvanus Osoro, Seneta wa Bungoma David Wakoli, pamoja na wabunge Nabii Nabwera (Lugari), Dick Maungu (Luanda), John Waluke (Sirisia) na Kakai Bisai (Kiminini), miongoni mwa wengine.

Ichung’wah alikubaliana na kauli za Wetang’ula, akionya kuwa wote waliohusika kupanga au kufadhili maandamano yenye vurugu, bila kujali nafasi yao ya kisiasa, watakabiliwa na sheria.

“Iwe wewe ni mbunge au la, ikiwa ulipanga au kufadhili ghasia hizo, utawajibika kisheria. Hata mimi, kama Kiongozi wa Wengi, sitasalimika. Hakuna aliye juu ya sheria,” alisisitiza.

Kauli hizi zilionekana kumlenga Mbunge wa Naivasha Jane Kihara, ambaye alikamatwa hivi karibuni kuhusiana na maandamano hayo.

Kupitia kwa jopo lake la mawakili wakiongozwa na Wakili Mkuu Kalonzo Musyoka na Ndegwa Njiru, Kihara amekana mashtaka hayo na kuyaita ya kisiasa.

Hata hivyo, Ichung’wah hakusita, akisisitiza kuwa wale waliowachochea vijana kupora mali na kuharibu vitu lazima wawajibike.

“Acheni kulia. Kama uliwaambia vijana wapore maduka, wachome vituo vya polisi au waharibu mali, ujitwike msalaba wako. Waombe wafadhili wako wa kisiasa wakusaidie kuubeba,” alisema.

Mbunge huyo pia aliwahimiza wakazi wa Bonde la Ufa kupinga juhudi zozote za kuchochea migawanyiko ya kikabila, akiwakumbusha wasirudie makosa ya ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007/08.

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved