
Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang’ula akihutubia hafla ya kisiasa katika eneo la Bogusero, kaunti ya Kisii Alhamisi/MOSES WETANG'ULA FACEBOOK
Akizungumza katika eneo la Bogusero, Kaunti ya Kisii Alhamisi, Bw. Wetang’ula alisema serikali ya Rais William Ruto imefungua miradi iliyokwama, kupanua nafasi za uwezeshaji vijana na wanawake, na kuimarisha sekta muhimu za kilimo na elimu.
“Serikali imejitolea kuinua sekta zote za uchumi. Rais ana dhamira ya kuinua viwango vya elimu kwa kuajiri walimu zaidi, kufungua barabara mpya na kuongeza tija ya kilimo,” alisema Spika.
Alisisitiza kuwa uwezeshaji wa vijana ni kipaumbele, akifichua kwamba vijana 70 katika kila wadi watapatiwa Sh50,000 kila mmoja kusaidia miradi ya biashara ndogo na za kati.
“Hii itakuza uhuru wa kiuchumi na kusukuma mbele maendeleo ya taifa. Hakuna jamii itakayobaguliwa katika mpango mkubwa wa maendeleo ya kiuchumi wa nchi hii,” akaongeza.
Bw. Wetang’ula pia aliwataka wanasiasa kuwa wavumilivu na wastahimilivu katika siasa za kitaifa. “Turuhusiwe kufurahia haki zetu za kikatiba bila matusi, kejeli au vitisho.
Viongozi lazima wapime maneno yao iwapo kweli tunataka taifa lenye uongozi bora,” alionya.
Katika mkutano huo, aliandamana na Kiongozi wa Wengi katika Seneti, Bw. Aaron Cheruiyot, aliyewataka viongozi wa jamii ya Kisii kuachana na siasa za kikabila.
“Maneno yetu lazima yawe ya kujenga amani na mshikamano. Hakuna mtu ana mamlaka ya kuzuia wengine kusafiri au kufanya siasa. Wakenya wataamua kwa kura, na tutavuka daraja la 2027 tutakapofika,” alisema Cheruiyot.
Kiongozi huyo alimtetea Rais Ruto akisema uongozi wa urais unahitaji nguvu na uungwaji mkono wa kitaifa.
“Ninapoangalia wapinzani wetu, najiuliza kama wana uwezo wa kufikia ari na jitihada tulizo nazo. Kenya Kwanza itaendelea kuzuru nchi nzima kuhubiri amani na kujenga mazingira bora ya maendeleo,” akaongeza.
Naye Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Kisii, Bi. Dorice Donya, alisifu miradi ya uwezeshaji inayoendeshwa na serikali, akisema inadhihirisha matunda ya Ajenda ya Mageuzi ya Kiuchumi ya Bottom-Up.
“Tumeweka malengo sahihi. Rais Ruto anaiongoza nchi katika mwelekeo ufaao,” alisema Bi. Donya.
Viongozi wengine akiwemo Mbunge wa Emurua Dikirr, Bw. Jonah Ngeno, Kiranja wa Wengi Silvanus Osoro, na Seneta Mteule Essy Okenyuri, walitoa wito kwa jamii ya Gusii kutumia fursa za maendeleo chini ya serikali ya sasa badala ya kuzama upinzani.
Miongoni mwa walioungana nao ni wabunge Japheth Nyakundi (Kitutu Chache Kaskazini), Alfa Miruka (Bomachoge Chache), Steve Mogaka (West Mugirango), Jerusha Momanyi (Mwakilishi wa Kike Kaunti ya Nyamira), pamoja na Mbunge Mteule Rene Nyakerario.