logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Nyota wa Zamani wa Arsenal Akana Mashtaka Mazito ya Ubakaji

Kesi yake itasikilizwa Novemba mwaka ujao huku akiwa huru kwa dhamana.

image
na BBC NEWS

Kandanda17 September 2025 - 16:11

Muhtasari


  • Thomas Partey, mchezaji wa zamani wa Arsenal na sasa wa Villarreal, amekana mashtaka matano ya ubakaji na moja la unyanyasaji wa kijinsia katika Mahakama Kuu ya Southwark, London.
  • Kesi hiyo inahusu matukio ya 2021–2022, na Partey ameachiliwa kwa dhamana hadi Novemba mwaka ujao.

LONDON, UINGEREZA, Jumatano, Septemba 17, 2025 — Mchezaji wa zamani wa Arsenal, Thomas Partey, amekana mashtaka ya kubaka wanawake wawili na kumdhulumu kimapenzi mwanamke wa tatu.

Kiungo huyo wa kati kutoka Ghana alikana mashtaka matano ya ubakaji na shtaka moja la unyanyasaji wa kijinsia alipofikishwa katika Mahakama Kuu ya Southwark, London.

Thomas Partey/THOMAS TEYE PARTEY FACEBOOK

Madai hayo yaliibuka kati ya mwaka 2021 na 2022, wakati nyota huyo mwenye umri wa miaka 32 alikuwa akicheza mara kwa mara kwenye Ligi Kuu ya Uingereza.

Alishtakiwa siku nne baada ya kuondoka klabuni Arsenal kufuatia kumalizika kwa mkataba wake mwishoni mwa Juni.

Hakimu alimweka huru Partey kwa dhamana hadi kesi yake itakapoanza Novemba 2, mwaka ujao katika mahakama hiyo hiyo.

Partey alithibitisha jina lake kabla ya kujibu mashtaka yote kwa kusema “sio hatia.”

Mchezaji huyo, ambaye sasa anachezea klabu ya Villarreal nchini Hispania, tayari alikuwa Uingereza kwani timu yake mpya ilicheza dhidi ya Spurs katika Ligi ya Mabingwa Ulaya siku ya Jumanne.

Alitokea benchi na kucheza kama mchezaji wa akiba, lakini Villarreal walishindwa 1-0.

Masharti ya dhamana hayamzuii Partey kucheza kandanda, lakini anapaswa kuwajulisha polisi masaa 24 kabla ya kusafiri kimataifa na pia amekatazwa kuwasiliana na waathiriwa wanaodaiwa.

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved