
SERIKALI kupitia kwa mkuu wa Uchumi Ubunifu na Miradi Maalum ya Rais, Dennis Itumbi imelazimika kuomba msamaha kwa wanafunzi wa shule ya upili ya wasichana ya Butere kwa ghasia zilizosababisha wao kutupiwa vitoa machozi.
Akizungumza kwenye runinga ya Citizen, Itumbi alisema kwamba
zogo lililojiri katika hafla ya kitaifa ya michezo ya kuigiza kwa shule ambapo
wasichana hao walijikuta katikati ya fujo na kutupiwa vitoa machozi na maafisa
wa polisi ni jambo ambalo halikuhitajika kutokea.
Itumbi aliwaomba msamaha wasichana hao, akisema kwamba
msamaha huo pia unatoka kwa serikali maana yeye ni mmoja wa watu wanaowakilisha
sehemu ya serikali katika suala zima la ubunifu.
Itumbi alibanwa na kulazimika kuomba msamaha huo baada ya
mchekeshaji Njugush kuhoji kwa nini serikali bado haijaona kama ilifanya kosa
kuwavuruga wanafunzi hao kisa tu tamthilia yao yenye utata ya Echoes of War.
"Nichukue fursa hii
kwa mikono na heshima zote za serikali kuwaomba radhi wasichana wote wa Butere
Girls kwa mabomu ya machozi waliyopigwa. Ninaomba radhi kwa dhati," Itumbi alisema.
"Pamoja na msamaha
wangu unakuja nguvu kamili ya serikali kwa sababu ninawakilisha sekta ya
serikali kwa uchumi wa ubunifu. Hatusikitiki tu kwa mabomu ya machozi lakini
pia kwa kutosimamia hili hadi mwisho. Naahidi kukaa na timu yangu na kuja na
suluhisho la nini kifanyike."
Itumbi zaidi aliomba radhi kwa wasichana kukosa fursa yao kuu
ya kucheza mchezo wao wa Echoes of War katika ngazi ya kitaifa, fursa ambayo
wamekuwa wakiifanyia kazi.
Tamthilia ya Echoes of War ilizua minong’ono kote mitandaoni
baada ya kile kilichosemekana kuwa ni juhudi za serikali kutotaka ichezwe.
Echoes of War
iliandikwa na aliyekuwa katibu mkuu wa UDA, Cleophas Malala ambaye amekuwa
akiipinga serikali tangu kuondolewa kwenye wadhifa huo.